PEMBE NDOGO YA DANIEL 08.

PEMBE   NDOGO   YA   DANIELI   8

(SOMA  DANIELI  8  YOTE)
Ninapenda kuwakaribisha katika muendelezo wakujifunza neno la Mungu hasa katika unabii wa Daniel, kwanza ninapenda kuweka wazi jambo hili ,hatufundishi kwa kushambulia dhehebu au dini bali tunasema yaliyo kweli hasa ,kwahiyo usidhani kuna mabishano ya hoja ,hapana tunasema na kweka huru ukweli ili mtu mwenyewe asome ,alinganishe na kufanya uamuzi yeye mwenyewe ,jambo jingine ni kwamba MUNGU huwa anawapa taarifa watu wake kabla ya maafa kuwapata ,kwahiyo haya ni maonyo kwa watu wake kuhusu yale ambayo yanaendelea iliyatakapo tokea asiwepo mtu atakayesema Mimi sikuyasikia ,wala sikuambiwa ili hukumu itakapokuja kila mtu aseme HAKIKA HUKUMU ZAKO NI ZA HAKI NAZA KWELI .
Kwahiyo hatutoi mafundisho kwa kujaribu tunatoa ukweli kama ulivyo ,ni kweli unapoguswa lazima utafute njia ya kujitetea lakini kumbuka wokovu ni maamuzi yako ,muda Utakuja ambapo neno la Mungu halitaonekana tena ,ninacho kushauri usichoke kujifunza neno la Mungu omba Mungu akufunulie zaidi ,utabarikiwa na uzima wa milele uaambatana nawe.

Kumbuka kama tulivyoona kuwa Pembe  Ndogo  ya  Danieli  7 inawakilisha Ufalme wa  Papa.   Lakini  Pembe  Ndogo  ya Danieli 8 inaziwakilisha  falme  mbili  -----  Rumi ya  Kipagani na  Rumi ya Kipapa.  
 Ni sawa tu na lile Joka Kubwa Jekundu la Ufunuo 12 lenye vichwa saba na  pembe  kumi  ambalo linaziwakilisha  falme  zizo hizo  mbili.   Utazitofautisha kwa vitendo  vyake  tu.  
Mungu  haoni tofauti  yo  yote kati  ya  Rumi  ya Kipagani  na  Rumi  ya Kipapa.  
 Yesu  aliziita falme  zote  mbili "Chukizo la Uharibifu,"  yaani, Mamlaka Zinazowaangamiza  watu  wa Mungu (Mt. 24:15,22;  Dan. 9:27). Danieli  8  na  9  ni  kitu  kimoja;   Gabrieli  alishindwa  kuendelea  kumweleza  Danieli habari za Pembe  hiyo  Ndogo  ambayo  itawaua watakatifu  kiasi  cha kustaajabisha  kwa vile alikuwa  amezimia  (Dan.  8:24,27).  
Baada  ya  muda  kupita  Gabrieli  alimjia  tena  Danieli akamwambia anataka kumpa ufahamu wa njozi  ya  Danieli  8  ambayo  alikatisha kumweleza (Dan. 9:20-22).  Lakini kwa urahisi wa kuelewa tutachukua kila sura peke yake. Katika sura ya 8 kuna maono ya aina mbili  -----  Kondoo mume  mwenye  pembe mbili (Dan.  8:3,4) ambaye  anawakilisha Ufalme  wa Wamedi na Waajemi  (Dan.  8:20);   kisha akaona  Beberu  mwenye  pembe  mashuhuri  kati  ya  macho  yake  (Dan.  8:5-8)  ambaye anauwakilisha Ufalme wa Wayunani (Dan. 8:21).  Ile pembe mashuhuri ni mtawala wa kwanza  Iksanda  Mkuu  (Dan.  8:21).    Zile  pembe  nne  ni  majemadari  wake  wanne waliotawala baada  ya kufa kwake Iskanda  Mkuu (Dan. 8:22).   Cassander  alitwaa Jimbo la Magharibi;  Lysimachus Jimbo la Kaskazini;  Seleucus Jimbo la Mashariki (Siria  kwenda mashariki), Ptolemy  Jimbo  la Kusimi (Misri  na visiwa).  
 Falme hizo  za Kiyunani  zilipigana zenyewe kwa zenyewe;  hatimaye Seleucus akachukua eneo lote la mashariki,  kaskazini, na  magharibi  baada  ya  kuwashinda  wenzake.  

 Ni  katika  pembe  (ufalme)  ya  Seleucus ilimotokea Pembe ile Ndogo ambayo inaiwakilisha  Rumi ya Kipagani, na hatimaye Rumi ya Kipapa (Dan. 8:9).  Kwa maneno mengine Ufalme wa Warumi ulitokea katika eneo la Seleucus alilotawala.
 Hiyo ni kweli kijiografia na kihistoria. Sasa  tutaangalia mambo  machache tu  juu  ya kazi  iliyofanywa na  Pembe  hiyo  Ndogo ya Danieli 8.   Mungu  kwa  mkono  wa  Musa  alikuwa  amewaonya Waisraeli kuwa  atawaletea taifa ambalo lugha yake hawaijui, litawazingira, watakula  watoto  wao;    hayo  yalitokea mwaka wa 70 B.K.
majeshi ya  Warumi  yalipouzingira  Yerusalemu  na  kuuharibu  kabisa pamoja  na  hekalu  lake  (Kum.  28:49-57;  Dan.  9:26,27;  Mt.  24:15-20;    Luka  21:20-24). Ukatili wa falme hizo zinazowakilishwa  na  "mfalme  mwenye  uso  mkali",  yaani,  katili, umedokezwa (Dan. 8:23,24). Wayahudi walijua Kiyunani lakini sio Kilatini.  Agano  jipya liliandikwa  kwa  Kiyunani,  lugha  ya  Dola  ya  Wayunani.  
 Falme  zote  mbili,  Rumi  ya Kipagani  na  Rumi  ya  Kipapa  zilitumia  hila  katika  kutawala  kwao  (Dan.  8:25).  Soma Historia ya Kale.  Mpaka hapo ni mambo ya jumla.  Sasa na tuangalie vitendo vya falme hizo kwa uchache tu:

RUMI YA KIPAGANI
:  

Pembe Ndogo ilikua sana kuelekea nchi ya uzuri,  yaani,  Palestina (Dan. 8:9).  Palestina  ilichukuliwa  na  kuwa  sehemu  ya Rumi ya Kipagani  mwaka 63 K.K.  "Jeshi la mbinguni" ni  watu  wa  Mungu,  "nyota"  ni  viongozi  wa  dini  (Dan.  8:10:    Ufu. 1:20).  "Kuangusha chini na kukanyaga" ni kuangamiza  au  kuua.    Ufalme  huu  ulitimiza hayo mwaka 70 B.K. ulipouangamiza Mji  wa Yerusalemu,  kisha katika karne  ya pili uliua wakristo  wengi  chini  ya  Kaisari  Diocletian  wa  Rumi.  

Hata  kabla  yake  wakati  wa  Nero mauaji  ya Wakristo yalifanyika.   Historia  inaweka  idadi  ya  waliouawa  na  Rumi  ya Kipagani takriban milioni  3.  "Patakatifu  pakaangushwa  chini" ni kuliharibu  hekalu  mwaka 70 B.K. (Dan. 8:11).  "Mkuu wa Jeshi"  au  "Mkuu  wa  wakuu"  ni  Kristo  mwenyewe  (Dan.  12:1. Ufu.  12:7,8;   Yoshua  5:13-15;  Ufu.  1:5).    Neno  "malaika"    maana  yake  "mjumbe". Linaweza kutumika  kwa  Kristo  na  kwa  viumbe  wale  wa  mbinguni  tunaowaita  malaika (Ebr.  1:14),  au  kwa  "wachungaji"  (Ufu.  2:1,8,12,18;   3:1,7).    "Mikaeli"  ni  jina  la  Yesu anapokuwa Mkuu wa Majeshi ya  Malaika  (Amiri  Jeshi  wa  Jeshi  la  Bwana).    
Sauti  yake ndiyo itakayowafufua wafu  (Yoh.  5:25,28,29;   1  The. 4:16),  anaitwa  Malaika  Mkuu.    Huyo Pilato, Gavana wa Rumi ya Kipagani, alikabiliana naye ana kwa ana  kama  ilivyotabiriwa katika Dan. 8:11,25 (Yoh. 18:33-37; 19:1-3,10,11,23,19-22).   Alisulibiwa  juu  ya  msalaba wa Kirumi; alipigwa kwa mijeledi ya Kirumi, na kupigiliwa kwa misumari ya  Kirumi,  na kaburi lake likalindwa na askari wa Kirumi.  Unabii huo ulitimia mia kwa mia.

 RUMI  YA  KIPAPA:  

Tutaangalia  mambo  kadhaa  tu,  sio  yote.    Rumi  ya  Kipapa ili"iangusha kweli  hata chini" (Dan.  8:12).  Kweli ni nini?   Kweli ni Neno  la Mungu, kweli ni Sheria  ya  Mungu  (Amri  Kumi).    Soma  Yoh.  17:17;    Zab.  119:142.    Upapa umeikanyaga chini ya miguu yake Sheria ya  Amri Kumi kwa kufuta Amri ya  pili inayokataza ibada ya sanamu, na  kuweka  Jumapili  badala ya  Sabato  (Jumamosi)  kama  siku ya ibada  (Dan.  7:25; Ufu.  13:16,17).   Jumapili  katika  unabii  inaitwa  "Chapa  au  Alama  ya  Mnyama",  yaani, Alama ya Uwezo wa Mamlaka ya Papa.
 
 Sabato inaitwa Muhuri wa Mungu (Ufu. 7:1-4) au  "Alama  ya  Mungu"  (Eze.  9:4-11).  
 Martin  Luther  aligundua  makosa  (mafundisho potofu)  95.    Sasa  ni  zaidi  kuliko  hayo.    "Kukanyagisha  patakatifu  na  jeshi";    yeye hajaliangusha  jengo  la hekalu,  ila  amegeuza  mawazo  ya waumini  kumwelekea  yeye  badala ya Kuhani  Mkuu, Yesu  Kristo,  katika  Hekalu  la Mbinguni  kwa  kuanzisha  ukuhani  na misa (Ebr. 4:14-16;   3:1).    Kosa  lingine  ni lile  la kutumia  cheo  cha  Mungu  cha  "Baba  Mtakatifu" (Yoh. 17:11).  Muda  hautoshi  kuorodhesha  mafundisho  potofu  yanayoitwa  "mvinyo  ya ghadhabu ya uasherati wake" (Ufu. 14:8;  17:2).  Unafundisha Mapokeo badala ya Biblia (Mt. 15:3-9;   Marko 7:5-13).   Uliua  watakatifu  zaidi ya milioni  50 katika  kipindi  chake cha utawala  wa miaka  1260  (538-1798), kiitwacho  Zama  za Giza  (Dan.  8:24,25;  Mt.  24:21,22). Waliomo  katika  mfumo  huo  wa  utawala  wanaambiwa  watoke  (Ufu.  18:4,5).  Maana yake watoke katika kuabudu bila kufuata maagizo ya Mungu namna ambayo wanasema kuabudu ,hapa watu wote  kuanzia anayekalia kiti  cha  papa  hadi  mlei  wanatakiwa watoke katika huo mfumo maana mungu mwenyewe wanasema watoke .Na mamilioni watatoka kwa dhiki  kubwa  pamoja  na  kuuawa na wale  watakaobaki katika  mfumo  huo  (Ufu.  15:2;  20:4). Katika  Danieli  7:9,10 hukumu  ilifuatia  baada  ya  upapa kufanya  kazi  yake  kwa  miaka 1260.  Hapa pia tunaona hukumu ile ile ikirudiwa kwa maneno haya:  "Hata  nyakati    za jioni na asubuhi elfu mbili na  mia  tatu;    ndipo  patakatifu  patakapotakaswa"  (Dan.  8:14). hili somo nitalitolea Maelezo baada ya hili kuisha ,na somo la patakatifu litafuaata. Mpango wote wa wokovu umedhihirishwa katika Hekalu la duniani  na  lile  la  Mbinguni (Ebr. 8:1,2;  9:6,7;  Law.  16 yote;  Law. 23:27-32).  Tangu Sinai hadi  Yesu alipokata roho msalabani huduma hiyo iliendeshwa  na  makuhani  pamoja  na  kuhani  mkuu  na  kufikia mwisho wake (Kut. 25:8;  Mt. 27:50,51).
 Yesu  alipopaa mwaka 31 B.K. alikwenda moja kwa moja katika huduma ya chumba cha kwanza cha Hekalu la mbinguni (Ebr. 9:11,12) kama Kuhani Mkuu.
Siku  2300  za Dan.  8:14  ni  siku  za unabii, ni  sawa  na miaka  2300  (Eze. 4:6).   Zilianza kuhesabiwa wakati ule amri ya kuujenga upya Yerusalemu ilipotolewa mwaka  457  K.K. na  kukoma  1844  B.K.   Kutakaswa  kwa  Patakatifu  ni  kazi  ya  Hukumu  au  Utakaso  au Upatanisho aliyoanza kufanya Kristo mwaka 1844 katika chumba cha pili cha  Hekalu  la mbinguni  kinachoitwa  Patakatifu  pa  Patakatifu  (Ebr.  9:23-26;   Ufu.  11:19).    Akimaliza atatamka maneno ya kutisha sana yatakayoamua umilele wa kila mmoja wetu,  ama  kwa uzima wa milele, ama kwa  mauti  ya  milele, hapa ndipo uamuzi wako leo utakuamulia upande ambao utakuwa.  (Ufu.22:11,12).    Ndipo  atakuja  kuwachukua watu  wake  na  kuwaangamiza  waovu.   Waovu ni watu gani leo ,? kwa ufupi wote tumepungukiwa na utukufu wa. Mungu ndio maana tunarudi miguuni pake kwa kuangalia mapito aliyopita na kuenenda katika maagizo yake ,usikubali kuendeshwa na mwanadamu hasa kwa maisha ya kiroho mruhusu Mungu mwenyewe akuongoze kupitia neno lake.

 Somo  la  Patakatifu  litafuata baada ya kumaliza unabii huu wa Daniel hilo somo ni mhimu sana linaonesha nini kinachoendelea kwa kila mwanadamu leo ambacho kikimalizika tayari nafasi tena ya Rehema haitakuwa na nafasi ,kumbuka Mpendwa hii nafasi ya kupata neno la Mungu itakuja kuwa na ukomo wake hivyo shika sana kila unachopata kwa unabii huu (Amos8:11-14) Bwana akubariki Karibu kwa sura inayofuata.
Previous
Next Post »

1 comments:

Click here for comments
Unknown
admin
18 April 2024 at 12:28 ×

Bwana Yesu asifiwe!
nimejaribu kupitia masomo uliyoyaweka kwenye blog yako
Mungu akubariki maradufu
naweza pata no yako?

Congrats bro Unknown you got PERTAMAX...! hehehehe...
Reply
avatar