Chimbuko la Dhambi Katika mawazo ya watu wengi chimbuko la uovu na sababu ya kuwapo kwake ni chanzo cha utata mkubwa sana kwao. Wanaona matendo mabaya, pamoja na matokeo yake ya kutisha yaletayo misiba na maangamizi, nao huuliza kwamba mambo hayo yote yanawezaje kuwapo chini ya utawala wa yule Mmoja aliye na hekima, uweza, na upendo usio na kikomo. Ni jambo lisilowezekana kabisa kueleza chimbuko hilo la dhambi kwa kiasi cha kuweza kutoa sababu ya kuwapo kwake. Lakini kinaweza kufahamika kiasi cha kutosheleza kwa mambo haya mawili, chimbuko la dhambi na kuondolewa kwake hatimaye, ili kudhihirisha kwa ukamilifu haki na fadhili zake Mungu katika kuushughulikia kwake kote uovu huo. Dhambi ni kitu kinachojiingiza chenyewe, kuwako kwake hakuna sababu iwezayo kutolewa. Kama udhuru wo wote ungeweza kupatikana wa kuwako kwa dhambi hiyo, au sababu yo yote ingeweza kutolewa kwa kuwako kwake, basi, ingekoma kuwa dhambi. Maana ya dhambi tuliyo nayo peke yake ni ile iliyotolewa katika Neno la Mungu; yaani, [dhambi] ni uvunjaji wa Sheria [Amri Kumi - 1 Yohana 3:4, AJKK].Upendo wa Mungu dhidi ya Kiburi Sheria ile ya upendo [Amri Kumi - Mt. 22:35-40; Rum. 13:8-10; Yak. 2:10-12] ikiwa ndiyo msingi wa Serikali ya Mungu, basi, kule kuafikiana kabisa na kanuni zake za haki lilikuwa ndilo tegemeo la furaha ya viumbe vyote vilivyoumbwa. Mungu anataka huduma ya upendo toka kwa viumbe vyake vyote - yaani, ibada ile itokanayo na kuithamini tabia yake kwa kutumia akili zetu. Haufurahii utii unaotolewa kwake kwa kujilazimisha, tena yeye huwapa wote uhuru wa kufanya wapendavyo, ili waweze kumpa huduma yao ya hiari. Lakini alikuwako mmoja aliyechagua kuutumia vibaya uhuru wake. Dhambi ilianzishwa na huyo, ambaye, akiwa wa pili toka kwa Kristo, alikuwa amepewa heshima kubwa sana, naye alikuwa amesimama mahali pa juu sana pa mamlaka na utukufu miongoni mwa wakazi wote wa mbinguni. Kabla ya anguko lake, Lusifa [Lucifer = Nyota ya Alfajiri - Isa. 14:12, KJV] alikuwa Kerubi afunikaye wa kwanza, mtakatifu, na asiye na waa. Angalia Ezekieli 28:12-15. Lusifa angeweza kubakia katika upendeleo wa Mungu, akiwa anapendwa na kuheshimiwa na jeshi lote la malaika, akitumia uwezo wake mkuu kuwaletea furaha wengine na kumtukuza Muumbaji wake. Lakini, asema hivi huyo nabii, "Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako." Ezekieli 28:17. Kidogo kidogo, Lusifa akaanza kuingiwa na tamaa ya kujikweza mwenyewe. "Nawe ulisema … Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na Yeye Aliye Juu." Isaya 14:13,14. Badala ya yeye kumfanya Mungu aonekane kuwa ndiye kuliko wote katika mapenzi na utiifu wa viumbe vyake, ilikuwa ni jitihada yake Lusifa kuwashawishi watoe huduma yao pamoja na utii wao kwake yeye mwenyewe. Naye akiwa anatamani sana heshima ile ambayo Baba wa milele alikuwa amempa Mwanawe, mkuu huyo wa malaika akataka sana kujinyakulia mamlaka yale ambayo ilikuwa ni haki yake Kristo peke yake kuyatumia. Mwana wa Mungu alikuwa ndiye Mfalme wa mbinguni aliyetambulikana hivyo, akiwa na uweza na mamlaka kama Baba yake. Katika mashauri ya Mungu, Kristo alishiriki, ambapo Lusifa hakuruhusiwa hivyo kuingia katika makusudi ya Mungu. "Kwa nini Kristo awe mkuu kuliko wote"? akauliza yule malaika mwenye uwezo mwingi, "Kwa nini yeye anaheshimiwa kuliko mimi Lusifa?"Ajivika Usiri Shetani alikuwa amepewa heshima kubwa sana, na matendo yake yote yalikuwa na usiri, hata ikawa vigumu [kwa Mungu] kuwafunulia malaika wale hali halisi ya kazi yake. Mpaka hapo itakapofikia ukamilifu wake, dhambi isingalionekana kuwa ni kitu kibaya kama vile ilivyo. Mpaka wakati ule ilikuwa haina nafasi yo yote katika malimwengu ya Mungu, wala viumbe wale watakatifu hawakuwa na wazo lo lote kuhusu hali yake halisi, wala ubaya wake. Hawakuweza kutambua athari zake zitakazotokea kwa kitendo cha kuiweka kando Sheria ya Mungu [Amri Kumi]. Katika kuishughulikia dhambi, Mungu angeweza kutumia haki na kweli tupu. Shetani angeweza kutumia kile ambacho Mungu asingeweza kutumia yaani, kujipendekeza na udanganyifu. Hali ile ya kutokuelewana iliyosababishwa na mwenendo wake kule mbinguni, Shetani akailaumu Sheria [Amri Kumi] na Serikali ya Mungu [kuwa ndicho chanzo chake]. Akatangaza kwamba maovu yote yalikuwa ni matokeo ya utawala wa Mungu. Akadai kwamba lilikuwa ni lengo lake kuziboresha Sheria za Yehova. Kwa ajili hiyo, ilikuwa ni lazima kwamba aonyeshe sura ya madai yake, na kuonyesha utendaji wa mabadiliko yake aliyokuwa amependekeza yafanyike katika Sheria ile ya Mungu [Amri Kumi]. Kazi yake ni lazima imhukumu mwenyewe. Tangu mwanzo Shetani alikuwa amedai kwamba alikuwa hajafanya maasi yo yote. Ni lazima apewe muda wa kujifunua mwenyewe kwa kazi zake za uovu. Ulimwengu wote unapaswa kumwona laghai huyo akiwa amefuchuliwaRoho Ile Ile Roho ile ile iliyochochea maasi kule mbinguni bado inaendelea kuchochea maasi hapa duniani. Shetani ameendelea kushughulika na wanadamu kwa kutumia mbinu yake ile ile aliyoitumia kwa wale malaika. Kwa njia ile ile ya kuieleza vibaya tabia ya Mungu kama vile alivyofanya mbinguni, alipomfanya [Mungu] afikiriwe kuwa ni mkali tena ni dhalimu, Shetani alimshawishi mwanadamu kutenda dhambi. Na baada ya kufanikiwa mpaka pale, akatangaza kwamba vizuio vyote vya Mungu ambavyo vilikuwa si vya haki ndivyo vilivyosababisha mwanadamu kuanguka dhambini, kama vile vilivyomfanya yeye kuangukia katika maasi yale. Mungu alitoa ushahidi wa upendo wake kwa kumtoa Mwanawe pekee kufa kwa ajili ya wanadamu walioanguka [dhambini - Yn. 3:16]. Katika upatanisho huo tabia ya Mungu imedhihirika. Hoja ile yenye nguvu ya msalaba hudhihirisha kwa malimwengu yote kwamba, kwa vyo vyote vile, Serikali ya Mungu isingestahili kutupiwa lawama yo yote kutokana na njia ile ya dhambi aliyoichagua Lusifa.
Kama tulivyoona chanzo cha dhambi ni kujiinua kwa yule aliyekuwa malaika mkuu Lucifer ambae hatimaye alishindwa vita iliyotokea mbinguni akatupwa hapa duniani akaitawala dunia yote ndipo Yesu kristo akaja kutufilia msalabani ,Mipango wa shetani daima ni uharibifu wa kila namna akiri zetu sio jambo la kushangaza kwa leo jinsi alivyoteka wanadamu kwa njia hata ya mitandao akiri zimefungwa kutoka katika kutafakari neno la Mungu, tumshukuru Mungu kwa kukupatia huu Ujumbe jitenge MBALI na uovu wa ibilisi ,maadamu tu NEEMA ingalipo
Karibu kwa somo linalofuata.
Kama tulivyoona chanzo cha dhambi ni kujiinua kwa yule aliyekuwa malaika mkuu Lucifer ambae hatimaye alishindwa vita iliyotokea mbinguni akatupwa hapa duniani akaitawala dunia yote ndipo Yesu kristo akaja kutufilia msalabani ,Mipango wa shetani daima ni uharibifu wa kila namna akiri zetu sio jambo la kushangaza kwa leo jinsi alivyoteka wanadamu kwa njia hata ya mitandao akiri zimefungwa kutoka katika kutafakari neno la Mungu, tumshukuru Mungu kwa kukupatia huu Ujumbe jitenge MBALI na uovu wa ibilisi ,maadamu tu NEEMA ingalipo
Karibu kwa somo linalofuata.
ConversionConversion EmoticonEmoticon