AFAULU   MTIHANI   WA   AMRI   YA   KWANZA.


Karibu tena Mpendwa katika kujifunza neno la Mungu, leo kinaendelea na kitabu cha Daniel sura ya sita ambapo tutajifunza namna ambayo Mungu anavyowaongoza waendao katika kweli yake ,Karibu tujifunze .

(SOMA  DANIELI  6  YOTE)
Rafiki Mpendwa tumeendelea kuufunua unabii wa Daniel katika masomo ya hapo awali tukaona kuwa Katika Babeli  ya  zamani  na  Babeli  Mkuu  wa  mwishoe  inadhihirika  tabia  ile  ile  ya Shetani  ya  kuichukia  Sheria  ya  Mungu  [Amri  Kumi]  na  kuwalazimisha  watu  kutenda kinyume  na Sheria  hiyo.   Waliabudu miungu,  sanamu,  na  wafalme.  

Nimrodi ndiye muasisi wa mji wa Babeli  (Mwanzo 10:8-12).   Aliabudiwa  kama mungu Beli  (jua).  Beli  (Isa. 46:1) ni  mungu  mkuu  wa Wababeli na Waajemi, ni kifupi  cha "Baali".    Historia  inaonyesha kuwa wapagani tangu siku za Babeli waliabudu jua katika siku ile ya Jumapili.
Tumeona jinsi vijana wale wanne (Danieli 1) walivyojaribiwa juu ya  Amri  ya  Sita, isemayo, "Usiue" (Kut.20:13).  Kula vyakula  na kunywa vinywaji vinavyodhuru mwili ni kujiua polepole. Walishinda  mtihani  ule.   Pia tumeona  wale  vijana watatu  (Danieli  3)  walivyojaribiwa juu ya Amri ya Pili inayokataza ibada ya sanamu (Kut. 20:4-6);  walishinda mtihani ule  mgumu japo walitupwa motoni.
 Mungu alipendezwa kuwaokoa.  Pia tuligusia  juu  ya  kujaribiwa kwa Yusufu  kule  Misri  juu ya  Amri  ya  Saba,  inayosema,  "Usizini" (Kut.  20:14).  
Alishinda.  Sasa tunamkuta Danieli (Danieli 6) akijaribiwa juu ya Amri  ya  Nane,  isemayo,  "Usiibe" (Kut. 20:15).   Alishinda  bila  shida (Dan.  6:4);  alikuwa  mwaminifu.   Kisha  tulidokeza  kuwa mtihani mgumu kuliko  yote  wa  siku za  mwisho ni  juu ya Amri  ya Nne,  inayohusu  Sabato ya Mungu (Kut.20:8-11).  Kizazi cha Sayansi na Teknolojia kitaweka siku ya kupumzika nyingine  isiyokuwa  Sabato.  
Dunia  itagawanyika  katika  makundi  mawili  -----    hao wazishikao Amri [Kumi] za Mungu pamoja na Imani ya  Yesu, na wale wasiozishika,  japo miongoni mwao watakuwamo wanaomwamini Yesu.  
Kushika Amri Kumi za Mungu ni lazima uzishike zote (Kut. 20:3-17;  Yak.2:10-12).  "Dhambi ni uvunjaji wa Sheria [Amri Kumi]" (1 Yohana 3:4,). Tukirudi kule Babeli tunamkuta mfalme Dario  aliyempenda  sana  Danieli,  mtu  wa Mungu.   Kutokana  na  "roho  bora  iliyokuwa  ndani  yake  Danieli,  alimteua  kuwa  Waziri Mkuu wa Babeli.  
Jambo  hilo  liliwakasirisha  sana  mawaziri  waliokuwa  wanawania  cheo hicho.  Wakatafuta  njia  ya  kumwondoa  katika cheo  hicho kwa kuchunguza  utendaji  wake wa kazi na matumizi ya fedha za Dola ile  ya  Wamedi  na  Waajemi,  "halikuonekana  kosa wala hatia ndani yake" (Danieli 6:1-4). Wakakaa  kikao  cha  faragha.    Wakatafuta  mbinu  hii  na  ile  wasiweze  kuiona. Hatimaye wakasema, "Hatutapata sababu ya kumshtaki  Danieli  huyo,  tusipoipata  katika mambo  ya    Sheria  ya  Mungu  wake  [Amri  Kumi].    Naam,  wazo  hilo  likawa  zuri  na likakubalika kwa wote.   Tahadhari ikawa kwamba  wasiweke amri yo  yote itakayomshtua mfalme maana anampenda Danieli.  Wakazipitia  amri  moja  moja  wakaona  ya  kwanza inafaa.  
Lakini Danieli  hawezi  kukubali  kuabudu  mwanadamu,  maana  amri  hii  inasema,  "Usiwe na  miungu  mingine  ila mimi"  (Kut. 20:3).   Wakasema mfalme atagundua tu  kuwa tumemlenga Danieli,  rafiki yake.  
Mmoja  akatoa  wazo  kuwa  tumhusishe  mfalme.   Tuseme watu  wote  waombe kwa mfalme kwa siku thelathini tu;   atajisikia vizuri,  wala  hatajua kuwa tumemlenga Danieli.    Wakasema  sisi  tunajua  kwamba  Danieli  hatakubali  na  tutakuwa tumemnasa kabisa,  cheo  cha Waziri  Mkuu  kitamponyoka;  kitakuwa chetu.    Sawa?   Sawa!  Wakamwendea mfalme kwa hila na  kumshurutisha  kuitia  amri hiyo  muhuri wake.    Soma Danieli l6:5-9.   "Basi mfalme  Dario akayatia  sahihi  maandiko yale,  na ile marufuku"  (Dan. 6:9).  Sheria  ya  Wamedi  na Waajemi  haiwezi  kubadilika, yaani,  haiwezi  kubatilishwa ikiisha kutungwa mpaka itekelezwe kama ilivyo.Basi Danieli, alipojua ya  kuwa yale maandiko yamekwisha  kutiwa sahihi, akaingia nyumbani  mwake,  (na  madirisha  katika  chumba  chake  yalikuwa  yamefunguliwa kukabili  Yerusalemu)" (Danieli 6:10).   Je!   aliomba  kimya  kimya  ili  watu  wasisikie  anaomba kwa nani?  "Wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za  Mungu  wake"  (Dan. 6:11).  
Alikuwa  anaomba  kwa sauti  kubwa  wanasikia  dua  anayotoa  kwa  Mungu  wake.   Ni ujasiri ulioje  mbele  ya kifo  kibaya  cha kuliwa  na simba!   Yesu  ameahidi  kwamba "kila  mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za  Baba  yangu  aliye  mbinguni"  (Mt. 10:32). Mkiri YESU mbele za watu naye atakukiri kwa MUNGU baba.
 Danieli alipokuwa anamkiri  Kristo  waziwazi  hata  mbele  ya  kifo  mbingu  yote ilikuwa  inaangalia  kila  kitu  kwa  makini  sana  na  kujiandaa  kumlinda.  Wengi  wetu tungekuwa tunaomba kimoyomoyo ili watu  wasije  wakatusikia  na  tukahatarisha  maisha yetu.   Matokeo  yalikuwaje  pamoja  na  juhudi  ya  mfalme  kutaka  amri  ile  isitekelezwe? "Wakamtupa katika tundu  la simba"  (Dan. l6:16).   Wakajipongeza  kuwa  njama  yao juu ya Danieli imefanikiwa kabisa na hawatamwona tena.
 Mfalme  alikuwa  na  imani  na  Mungu  wa  Israeli,   ijapokuwa  alikuwa na wasiwasi sana juu ya  usalama  wa  maisha  ya  rafiki  yake  Danieli,  alipoona  wamemtupa  katika  tundu  la simba. Akasema maneno haya, "Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya" (Dan. 6:16).  Mfalme hakulala usiku kucha akifikiria jinsi simba wanavyomrarua  vipande vipande  rafiki  yake;   akijilaumu  kwa  nini  hakugundua  njama  ya  mawaziri  wale waliomwonea wivu Danieli. Je!   simba  wale  wenye  njaa  kibao  walimla  Danieli,  Shahidi  wa  Yesu?    Mfalme akaenda kwenye tundu lile la  simba, akilia kwa huzuni, "Ee  Danieli, mtumishi wa Mungu aliye  hai,  je!   Mungu  wako,  unayemtumikia  daima,  aweza  kukuponya  na  simba  hawa [wenye  njaa]?"   Danieli  akamjibu mfalme,   "Mungu wangu  amemtuma malaika  wake, naye ameyafumba  makanwa  ya  simba  nao  hawakunidhuru"  (Dan.  6:21,22).  
 Simba  wale wakawa bubu;   makucha yao hayakufyatuka, wala  hawakuwa na ari  yo  yote  ya kumrukia. Mfalme  akaagiza  wamtoe.   Amri  ya  Wamedi  na  Waajemi  isiyobadilika  ilikuwa imetekelezwa lakini bila matokeo yaliyokusudiwa.  Akatoa amri nyingine  isiyobadilika  ili itekelezwe mara  moja.    Akaamuru waliomshtaki kwa  kijicho  chao  watupwe mle  mle,  "wao, na watoto wao, na wake zao" (Dan. 6:24).    Nini  kilitokea?    "Wale  simba  wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika  chini  ya  tundu"  (Dan.  6:24). Wivu  au  kijicho  kina  mshahara  wake!   Wengi  wanatafuta  njia  ya  kuwang'oa  wenzao kwenye  vyeo  vyao  kwa  kupeleka  mashtaka  ya  uongo  au  kutega  mitego  ya  hila  ambayo huwa vigumu sana kujinasua.  Mungu anaouna uovu wote huo. Wahenga walisema,  "Mchimba shimo  hutumbukia  mwenyewe."    Biblia  inasema, "Mwenye  kuchimba  shimo  atatumbukia  ndani  yake"  (Mhu.10:8).    Siku  zile  za  Esta Hamani akamwonea wivu au  kijicho  Mordekai.   Kwa siri  akachonga mti  mrefu  sana  wenye ncha kali wa kumtundikia Mordekai,  mtu wa Mungu aliyekuwa  hana hatia yo yote kama Danieli.   Matokeo?   Alitundikwa  mwenyewe  kwenye  mti  ule ule  aliouchonga  kwa  mikono yake (Esta 7:

KWANZA Mfalme  Dario  alimpenda  Mungu  wa  Danieli.    Mungu  naye  akampenda  mfalme huyo.   Akamtuma Gabrieli  kumthibitisha katika ufalme  wake  (Dan.  11:1).   Wafalme  wengi wangeiga  mfano  wa  mfalme  huyu  katika  kuwasaidia  na  kuwatetea  watu  wa  Mungu wanaowekewa mitego ya hila ili kuwaangusha.  Mungu  atawabariki  wafalme  kama  hao. Danieli  akashinda  mtihani  ule  mgumu  wa  kuitetea  Amri  ya  Kwanza.    Mfalme akawaandikia watu wa mataifa  yote watetemeke mbele za Mungu  wa Danieli.  Akasema, "Yeye  huponya  na  kuokoa,  hutenda  ishara  na  maajabu  mbinguni  na  duniani,  ndiye aliyemponya  Danieli  na  nguvu  za simba"  (Dan. 6:27).   Mungu  anasema,  "kwa  maana wao wanaoniheshimu  nitawaheshimu, na wao wanaonidharau watahesabiwa kuwa  si kitu (1 Sam.  2:30).   Danieli  akafanikiwa  chini  ya  wafalme  wawili  (Dan.2:28).   Vijana  /na watu wazima wote  leo wangeiga kielelezo cha Danieli.

Leo YESU anaita kwa wale wote watakao mpokea hata waacha kamwe hata mmoja (YOHANA 6:37)anashangaa pia kwa kuna wanadamu aliowafia hawampokei mpaka anauliza leo kwako ( YOHANA 5:40) kwamba hatutaki kumfuata atupe uzima bure ,rafiki yangu toa maisha yako kwa YESU ndiye pekee aliye na uzima naye atakuongoza katika uzima tele.
Usisite kuuliza maswali ,ukihitaji kujiunga kwaajili ya kujifunza zaidi Karibu kwa kanisa la MUNGU kanisa la waadventista wa Sabato popote utakapo kuwa utajifunza zaidi MUNGU akubariki.
Previous
Next Post »