USIKU WA MWISHO KWA MWANADAMU

Karibu tena ndugu Mpendwa tunapoendelea na kujifunza unabii wa neno la Mungu kupitia kitabu cha Daniel ,kiukweli kuna mambo mengi katika kitabu ambayo ni fundisho na mhimu sana kwa wokovu wetu .

ninakuarika usome hii sura
 (SOMA  DANIELI  5  YOTE)
Tinaangalia jinsi usiku mmoja unaweza kufuta historia ya mamia ya siku ,lakini hii natokea kwa sababu ipi ? fuatilia kwa makini somo hili utaelewa vizuri sana , sikia hili neno "Mpumbavu amesema moyoni,   Hakuna Mungu;   Wametenda uovu  wa ufisadi  na kuchukiza,   Hakuna  atendaye  mema"  (Zab.53:1).  
Watu wanaopenda kufanya  dhambi huamua  kumfutilia mbali Mungu  katika  mawazo  yao, mafundisho yao, na maisha yao.  Biblia inasema huo ni upumbavu.  Kwa sababu Mungu yuko kweli, na watu kama hao watawajibika  kwa  vitendo  vyao  viovu.  
 Lakini  jambo  la kusikitisha  ni  kwamba  hatujifunzi  kutokana  na  yale  yaliyowapata  watangulizi  wetu. Tunataka kujionea wenyewe. Siku moja mfalme Belshaza (mjukuu wa Nebukadreza) alifanya karamu kubwa ya ulevi  kwa  ajili  ya  wakuu  wake  elfu.  Hakujua  kwamba  karamu  yake  hiyo  ilikuwa  ya mwisho,  na  ya  kwamba  Mungu  wa  mbinguni  alikuwa  ameiona  hata  kabla  haijafanywa (Yer.  51:37-40,57-58).  
 Na  usiku  ule  karamu  ile  ikawa  ya  aina  yake;    lakini  wahusika hawakuweza kuamka asubuhi yake;  walikuwa maiti.  Belshaza hakujifunza kutokana  na mambo yaliyompata babu yake Nebukadreza (Dan. 5:18-23).  Alikuwa anajua yote hayo lakini  kwa  kiburi  kabisa akafanya yaliyomchukiza Mungu  wa  Mbinguni.  Je , hata sisi leo tunafanya mabaya kwa kujua au la ?

Makosa makubwa aliyoyafanya ni haya:

1- Kosa lake la kwanza ni kutumia vyombo vitakatifu kunywea pombe  (Dan.  5:1-3).
Hakuweka  tofauti  kati  ya  vyombo  vya  kawaida  vya  kutumia  na  vyombo  vitakatifu vinavyotumika  kwa  kazi  maalum  ya  Mungu.   Jinsi  gani  siku  hizi  wachungaji hawawafundishi  washiriki  wao  kuweka  tofauti  hiyo?    "Makuhani  [wachungaji]  wake wameihalifu  sheria  yangu  [Amri  Kumi],  wametia  unajisi  vitu  vyangu  vitakatifu; hawakuweka  tofauti  ya  vitu  vitakatifu  na  vitu  vya  kutumiwa  sikuzote;  wala hawakuwafundisha watu  kupambanua  vitu vichafu [kama  nguruwe, panya,  na kadhalika] na  vitu  vilivyo  safi  [kama  ng'ombe,  mbuzi,  kondoo],  nao  wamefumba  macho  yao, wasiziangalie  Sabato  zangu, nami  nimetiwa  unajisi  kati  yao"  (Eze.  22:26).    Kutokutambua vitakatifu ni kosa la kufisha.    Sabato  [Jumamosi]  ni takatifu (Mwa.2:2,3;   Kut. 20:11;  Isa. 58:13,14).   Jumapili  si  takatifu;   ni  siku  ya  kazi  (Eze.  46:1).    Siku  ya  ibada  aliyoiweka Mungu  kwa  wanadamu  wote  ni  Sabato  [Jumamosi]  na  itakuwa  hivyo  milele  zote  (Isa. 66:22,23).    Zaka  (sehemu  ya  kumi ya  mapato yetu)  ni takatifu (Law. 27:30-33).    Kuitumia kwa  matumizi  yetu  ya  kawaida  ni  kumwibia  Mungu  (Mal.3:8-11).    Wevi  hawataurithi ufalme  wa  Mungu  (1  Kor.  6:9,10).   Kumtegemea mchungaji wako  badala  ya  kusoma  Biblia mwenyewe ni hatari kubwa!

2- Kosa lake la pili ni kunywa divai [pombe] (Dan. 5:4a).  
 Tulijifunza  katika  somo  la kwanza lililohusu vyakula na  vinywaji kwamba pombe inaudhuru  sana mwili wetu, na ya kwamba  wale  wanaouharibu  mwili  wao  kwa  pombe  au  kwa  njia  nyingine  yo  yote wataharibiwa (1Kor.  3:16,17).  Pombe  ina sumu ya alkoholi  ambayo inaathiri  mishipa ya fahamu,  ubongo,  moyo,  nyama  za mwili,  na kadhalika.   Sio  suala  tu la  kulewa  linalohusika, bali  ni  ile  sumu  iliyomo.   Wengi  hata  wakinywa  pombe  nyingi  hawalewi;    lakini  sumu inafanya kazi  miilini  mwao na kuiharibu.  
 Hivyo wale  wasemao kunywa  pombe  kidogo tu wasingeweza kusema hivyo kuhusu sumu ya panya.  Sumu kidogo tu yatosha kuua mtu au kuuathiri  mwili (Mithali  23:29-35).   Biblia  inailinganisha sumu iliyomo  katika  pombe  na sumu ya nyoka aitwaye "fira" (Mithali 23:31,32).  Ni sumu mbaya  sana.    Biblia  inasema walevi [wanaolewa na wasiolewa] hawataurithi ufalme wa mbinguni (1Kor. 6:9,10).

3- Kosa la  tatu  la  Belshaza  ni  lile  la  kuisifu  miungu  badala  ya  Mungu  wa  mbinguni (Dan. 5:4b).  

Neno  lasema,  "BWANA asema hivi,  Mwenye hekima asijisifu  kwa sababu ya  hekima  yake,  wala  mwenye  nguvu  asijisifu  kwa  sababu  ya  nguvu  zake,  wala  asijisifu kwa sababu ya utajiri  wake;    bali  ajisifuye  na  ajisifu  kwa  sababu  hii  ya  kwamba ananifahamu  mimi,  na  kunijua,  ya  kuwa  mimi  ni  BWANA,  nitendaye  wema,  na hukumu,  na  haki,  katika  nchi;   maana  mimi  napendezwa  na  mambo  hayo,  asema BWANA"  (Yer.9:6).  
Si  kwamba  Belshaza  alikuwa  hamjui  Mungu  wa  mbinguni alipokuwa anaisifu miungu yake pamoja na  wakuu  wake,  kilikuwa  ni  kiburi  chake  sugu kilichomfanya afanye hivyo.  
Je! wewe unamsifu nani?

Wakati sherehe imefikia kilele chake, wamelewa na kuanza kusifu  wanawake  na miungu  yao,  kiganja  cha  mkono  kisichotoka  damu  kikaanza  kuandika  ukutani.    Jasho jembamba likawatoka.  Pombe yote ikayeyuka kichwani.  Hofu kuu  ikawashika,  wasijue la  kufanya.   Wataalam  wakaitwa  ili  wayasome  maandiko  yale;   hawakuweza.   Ndipo malkia,  mke  wa Nebukadreza, akaingia na kuwaambia habari  za  Danieli  jinsi alivyomtafsiria ndoto babu yake.  Danieli akaitwa.   Akamshutumu  Belshaza  kwa  kiburi  chake,  licha  ya kujua  fika  yaliyompata babu  yake.    Akasoma maandiko yale  ukutani:  
 "MENE (HESABU), MENE  (HESABU),  TEKELI  (MIZANI),  NA  PERESI  (MGAWANYO).   Na  tafsiri  ya maneno  hayo  ni  hii;   MENE,    Mungu  ameuhesabu  ufalme  wako  na  kuukomesha. TEKELI, Umepimwa  katika  mizani  nawe  umeonekana  kuwa  umepunguka.    PERESI, Ufalme  wako  umegawanyika,  nao  wamepewa  Wamedi  na  Waajemi"  (Dan.5:25-28). Ilikuwa imetabiriwa mapema  kwamba milango  ya  kuingilia  mjini  itaachwa  wazi na  maji ya mto  yatakaushwa
   (Isa. 45:1;   44:27).
 Hivyo  ndivyo  alivyofanya  Koreshi  aliyeyaongoza majeshi ya Wamedi  na  Waajemi  usiku  ule.    Milango  ya  mto  haikufungwa  usiku  ule. Wakaingia  na  kumwua  mfalme na viongozi wake  waliokuwamo mle.   Ulikuwa ni usiku  wa mwisho kwao. Mungu  anayapima  mataifa  katika  mizani  na  kukomesha  ufalme  wao  kama apendavyo.  Vile vile anampima mtu mmoja mmoja katika mizani ile ya mbinguni (Amri Kumi) na kuandika mbele  ya jina lake "umepunguka"  au "umetimilika  katika yeye" (Kol. 2:10).   Hiyo  ndiyo  kazi  anayofanya  Kuhani  wetu  Mkuu,  Yesu  Kristo,  mbinguni  tangu mwaka wa 1844.  Karibu sana kesi ya kila mmoja wetu itakatwa kwa milele.    Akimaliza kazi  yake  ya  upatanisho  au  hukumu  atatamka  maneno  haya  ya  kutisha:    "Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu;   na  mwenye  uchafu na azidi kuwa  mchafu;  na mwenye haki na azidi  kufanya  haki;  na  mtakatifu  na azidi  kutakaswa"   (Ufu.22:11).    Hukumu  hiyo itakatwa kabla  ya  kuanguka  mapigo yale  7  ya  Ufunuo  16.  Katika  pigo la mwisho  atakuja kuwachukua watu wake na kuwaangamiza waovu wote. Mkulima yule tajiri aliyevuna mavuno mengi asijue pa kuyaweka, alifikiri kwamba atakuwa  na  maisha  marefu  sana  ya  raha  mbele  yake
 (Luka  12:1621).   Usiku  ule akajiambia mwenyewe,  "Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba  kwa miaka mingi;  pumzika  basi,  ule,  unywe,  ufurahi"  (Luka  12:19).    Maskini  yule,  alipolala usiku ule hakuamka, aliuawa.  Yule mlinzi  mtakatifu  asiyeonekana  aliyeandika  ukutani Babeli, akatamka kwa tajiri huyo maneno haya,  "Usiku huu wa leo wanataka roho yako!  Vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa  vya  nani?"  (Luka 12:20).  
Ndugu  yangu, leo  ndiyo  siku ya  wokovu  (2  Kor. 6:2).   Kesho si yako  (Yak. 4:13-16).   Amua  leo kumpokea  Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wako.   Achana na ulevi na  dhambi zote.   Ukimpokea  atakupa  uwezo wa kushinda dhambi (l Kor. 15:57; Yuda 24,25). Usiku wa mwisho duniani kwako na kwangu unaweza kuwa ni usiku huu  wa  leo. "Basi jiangalieni,  mioyo  yenu  isije  ikalemewa  na  ulafi,  na  ulevi  na    masumbufu  ya maisha haya, siku ile ikawajia  kama  mtego  unasavyo;   kwa  kuwa ndivyo itakavyowajilia watu  wote  wakaao  juu  ya  uso  wa  dunia"  (Luka  21:34,35).    Siku  moja  ulimwengu  wote unaojifurahisha katika anasa  mbalimbali za dhambi hautaweza  kuiona asubuhi; watakuwa maiti, hawatazikwa, wala kuliliwa  (Yer.  25:32-37).    Itakuwa  karamu  ya  mwisho  Mungu atakayowafanyia ndege.
 (Ufu. 19:17,18).
ndugu Mpendwa kwa namna ya pekee Mungu wetu huwa anatoa onyo kabula ya kutoa adhabu kwa jambo baya leo ni siku ambayo umebarikiwa kusikia neno hili ,nani ajuaye kesho yake ni YESU pekee na ni yeye anayekuita sasa mpokee utakuwa huru kutoka katika utumwa wa dhambi ,mruhusu MUNGU aingie NDANI yako atakuongoza katika uzima wa milele .

Ubarikiwe Karibu kwa somo linalofuata na Mwinjilist Fredrick sylvanus.
Previous
Next Post »