KIBURI KWA NENO NA MATOKEO YAKE.

Mpendwa ninakukaribisha tena katika siku ya leo katika mfululizo wa masomo kutoka katika kitabu cha Daniel ,leo tutaangalia jinsi kiburi juu ya neno la Mungu kinavyoleta athali na Hatari , ukizingatia masomo ya hapo awali tuliona kwamba shetani ndiye baba wa uongo ,ndiye anayejenga kiburi juu ya uzima wa milele , Bwana ashukuriwe maana anaweza kubadiri kila kitu. Hebu soma hii sura ilitwende kwa pamoja kwa hili somo 
(SOMA  DANIELI  4  YOTE)
 

Hivi unadhani kiburi hutokana na nini ,kwa ufupi kinatokana na nafsi, yaani,  umimi.  Kiini cha dhambi zote ni ule umimi (nafsi).  Unaweza  kujikweza  au unaweza  kujidhalilisha isivyopasa.   Mambo  yote  hayo mawili ni kiburi.   Mwenye  kujikweza anasema, "Mimi ni tajiri, mimi  ni msomi, mimi... mimi...."   Anajiona kuwa yu bora kuliko wengine  kwa  vile  alivyo  na  kwa  vile  anavyofanya.   Anayejidhalilisha  isivyopasa akipongezwa kwa kazi  nzuri aliyofanya, anasema,  "Si  kitu!    Sikufanya  la  maana!...."   Lakini moyoni  mwake  anajipongeza  kuwa  amefanya  vizuri  sana.   Yule  anayesoma  mioyo anaandika katika kumbukumbu kuwa hicho ni kiburi. Kiburi kilimwangusha Lusifa mbinguni  akapewa  jina baya  la Shetani
 (Isa.  14:12-15;  Eze. 28:14-17).  Wazazi wetu  Bustanini  Edeni  walidanganywa  na  Shetani  kuwa  wakila tunda lile lililokatazwa watakuwa  kama  Mungu.    Wakala,  wakajiona  uchi,  wakapoteza utukufu  walioumbiwa nao,  na  wazao  wao  wakawa  wamepungukiwa na  utukufu huo (Mwa. 3:3-7;   Rum.3:23).   Mungu  anachukia  sana  kiburi  kwa  sababu  nafsi  yetu  inataka kumwondoa katika kiti  chake  cha enzi  mioyoni mwetu  na  kukikalia  yenyewe (Mithali 6:1619).  Tulijifunza katika somo la kwanza (Danieli 1) kwamba miili yetu ni Hekalu la  Roho Mtakatifu.   Mtu  anayeiruhusu  nafsi  kutawala  moyo  wake  anamfukuza  Roho  moyoni mwake. Kama  kuna  vita  kali kuliko  zote  hapa  duniani  ni ile  ya kupigana na nafsi  yetu.  
Nafsi haifi kabisa;  inaweza kukandamizwa tu isijitutumue.  Kwa hiyo ni muhimu kuwa macho kila wakati ili isije ikajitutumua  juu  ya  Mungu  au  juu  ya  watu  wengine.  Paulo alikuwa na vita iyo hiyo.  Anasema,  "Ninakufa kila  siku"
 (1Kor.  15:31).    

Kwa  maneno  mengine, "naifisha  nafsi yangu  kila  siku," au  "napigana  na umimi  unaojiinua  ndani  yangu."   Kuweza kuidhibiti nafsi ni kwa njia ya kumruhusu  Kristo  kukaa  moyoni  mwetu,    "Nimesulibiwa pamoja na Kristo;  lakini ni hai;  wala  si mimi [si umimi wangu]  tena, bali Kristo yu hai ndani  yangu;    na  uhai nilio nao sasa  katika  mwili, ninao  katika  imani  ya  Mwana  wa Mungu, ambaye alinipenda akajitoa  nafsi yake  kwa ajili  yangu"  (Gal.  2:20).  
Nafsi  itaondolewa ndani yetu wakati wa parapanda ya mwisho  tutakapopewa  miili  ya  utukufu,  isiyokufa  (1  Kor. 15:51-53).  
 Ndiyo  maana  si  vizuri  mtu  kujisifu  kuwa  ameokoka,  maana  anaweza kuangushwa  na  nafsi  wakati  wo  wote  na  kupoteza  wokovu  wake  (1  Kor.  10:12;   Eze. 33:12-16;   Mt.  24:13).
  Kwanza   kule  kujisifu  kwenyewe  tu  ni  dhambi  ambayo  haina msamaha  mpaka  mtu  huyo  atubu  na  kujishusha  kiburi  chake  (Luka  18:9-14).
 Tunaruhusiwa kujisifia msalaba  wa  Kristo  tu uliotuletea ukombozi  sisi  tusiostahili (Gal.6:14). Sifa  zote  anastahili  kupewa  Mungu  kwa  lo  lote  tufanyalo  au  kwa  mafanikio  yetu (Yer.9:23,24). Sasa  tunamkuta mfalme  Nebukadreza  aliyekuwa ameuona  uweza  mkuu  wa  Mungu wa kuwaokoa wale vijana watatu katika tanuru ile ya  moto,  na  kukiri  kwamba  "hakuna Mungu mwingine awezaye kuokoa  namna  hii"  (Dan. 3:29),  akijitukuza juu  ya  Mungu  huyo kwa njia ya kiburi chake.
 Mji wa Babeli ulikuwa na utukufu mkubwa sana (Isa.  13:19a).  
Hakuna ufalme mwingine  duniani unaoweza  kuwa  na  utukufu  kama  ule.  Mungu alimpa ndoto ya sanamu iliyowakilisha falme zote zitakazotawala kuanzia wakati wake  mpaka Kristo atakapousimamisha ufalme wake (Danieli 2).  Kwa kiburi akapinga  mpango  wa Mungu kwa kusimamisha sanamu ya  dhahabu tupu  (dhahabu iliwakilisha ufalme  wa  Babeli) katika uwanda wa Dura na kutaka watu waisujudie kama tulivyoona kwa somo la hapo nyuma .  Kwa  kiburi  alimdharau  Mungu  wa mbinguni  kuwa  si kitu;  bali  kwamba  yeye  atadumu  milele pamoja  na ufalme  wake.   Aliishi na  watu  wa  Mungu  ili  ajifunze  juu  ya  Mungu  wa  Israeli;   vijana  wale  wanne  walikuwa fundisho kuu kwake.  Hakujali yote hayo. Mungu katika  upendo  wake  akamletea ndoto  ya  pili  ili  kumwonya  aachane na kiburi chake sugu (Dan. 4:4-17).  
Katika  ndoto yake aliona mti mrefu  uliokua mpaka mbinguni; wanadamu, wanyama, ndege  wote  walipata chakula chao  katika  mti  huo.   Kisha akamwona mlinzi mtakatifu akiamuru mti ule ukatwe kibaki kisiki tu kikapate umande wa mbinguni kwa nyakati (miaka)  saba.  
 Kwa nini?   "Kusudi walio  hai wapate  kujua ya kuwa  Aliye juu anatawala katika  ufalme  wa wanadamu,  naye  humpa amtakaye,  tena  humtawaza  juu yake aliye  mnyonge"  (Dan.  4:17).   Ni  wafalme  wangapi  wanaofahamu  kuwa  ni  Mungu aliyewaweka katika viti vya enzi wanavyovikalia? hata leo tunapoona vitisho vya Vita baina ya mataifa ni kwa sababu wanasahau kwamba ni MUNGU aliyeruhusu wawe viongozi .
(Rum.13:1-7;  1 Tim. 2:1-6). Wajibu wa Serikali  zote  za dunia ni  kusimamia  utekelezaji  wa Amri Sita  za mwisho katika zile Kumi (Kut. 20:12-17).  

Wanapofanya kazi yao hiyo  vizuri na kwa uaminifu na haki mataifa yao yanabarikiwa.   Wanapoingilia mambo yanayomhusu  Mungu (Amri Nne za kwanza - Kut. 20:3-11)  wanavuka mipaka  ya madaraka aliyowapa  na kustahili adhabu kutoka  kwa  Mungu.
Kumbuka kuwa  Biblia sio  kitabu cha siasa;  lakini kuinuka  na  kuanguka  kwa mataifa yote  ya  dunia  kumeelezwa humo.  
Ni  Mungu  anayetawala katika  falme  zote  za  wanadamu. Mungu anapima nyendo  za  mataifa  yote  duniani  (Zab.  66:7-8;    Zaburi  2;   9:17).   Ni  jambo la  kusikitisha  mno  kwamba  mataifa  yote  ya  dunia,  ukiwaondoa  watakatifu  waliomo, yataangamizwa vibaya siku ile  ya mwisho kwa kwenda kinyume  na madaraka aliyowapa Mungu.
 je ,wewe hapo ulipo unatenda haki kama kiongozi ?.
 (Ufu. 19:11-21). Danieli alipoitwa kuitafsiri ndoto ile ya  mfalme  "akashangaa  kwa  muda,  na  fikara zake zikamfadhaisha" (Dan.  4:19).   Kwa  nini  alifadhaika?  
 Kwa  sababu  ndoto  ile  ilimaanisha kwamba mfalme angefukuzwa mbali na  wanadamu  na  kula  majani  kama  ng'ombe  kwa miaka saba.  Kwa nini iwe hivyo?  Kwa sababu ya kiburi chake sugu.  "Nyakati [miaka] saba  zitapita  juu  yako;   hata  utakapojua  ya  kuwa  Aliye  juu  ndiye  anayemiliki  katika ufalme wa wanadamu, naye humpa yeye amtakaye, awaye yote" (Dan.  4:25).    Miezi  12 baadaye, "alikuwa akitembea ndani ya jumba la kifalme katika Babeli.   Mfalme  akanena, akasema, Mji huu sio  Babeli  mkubwa  nilioujenga  mimi,  uwe  kao  langu  la  kifalme,  kwa uwezo  wa  nguvu  zangu,  ili  uwe  utukufu  wa  enzi  yangu?"  (Dan.  4:29,30).
Unaona alivyokuwa anajisifu ?  Pale  pale tangazo likatolewa kutoka mbinguni kuwa ufalme  wake umeondoka kwake na atakaa na wanyama akila  majani kama ng'ombe  kwa miaka  saba mpaka  atakapojifunza  kumtambua Mungu wa mbinguni.  Mafunzo ya miaka saba kukishusha kiburi sugu!  Fikiria hilo! Mungu  na  ashukuriwe!   Nebukadreza  alijifunza  kwa  njia  ya  aibu  sana  (ya  kuwa mwehu) kwa miaka saba mizima.  Alitoka akiwa kiumbe kipya;  akakitubia  kiburi  chake sugu na kuanzia  hapo  akaanza  kumtukuza  hadharani  Mungu  wa  mbinguni  (Dan. 4:34,35).
 Ufalme wake akarudishiwa.  Ushuhuda wake mbele za watu
ameutoa mwanzo wa Sura hii ya 4.  "Mfalme Nebukadreza, kwa watu  wa  kabila  zote,  na  taifa  zote,  na  lugha  zote, wanaokaa katika dunia yote;   Amani iongezeke kwenu.  Mimi  nimeona vema  kutangaza habari  za  ishara  na  maajabu,  aliyonitendea  Mungu  aliye  juu.   Ishara  zake  ni  kubwa kama nini!  na maajabu yake yana uweza kama nini!   ufalme  wake  ni  ufalme  wa  milele;  na mamlaka  yake ni ya  kizazi  hata kizazi"  (Dan.  4:1-3).  Siku  moja  wale watakaookolewa watakutana na Nebukadreza mbinguni.  Atawasimulia vizuri kisa chake.
Ni wangapi  ambao  Mungu anapozungumza nao  katika Neno lake  wanakaza  shingo zao  kwa  kiburi  na  kuyatukuza  mawazo  yao  juu  ya  Mungu  na  kufanya  kinyume  na maagizo yake?  Je,  wako  tayari  kupelekwa  porini  na  kula  majani  ili  wajifunze?    Hilo  ni zoezi kali mno.  Je! Mungu atanivumilia  mpaka  lini  asiukate  mti  wangu?  
(Luka  13:6-9).  Yatupasa kutubu;  la sivyo tutaangamizwa  (Luka  13:1-5).  Je, umewahi kufikilia juu ya kile ulichonacho unadhani ni nani aliyeruhisu ukipate ,je unamkumbuka Mungu kwa kukupatia usiseme ni kwaakiri zako maana pasipo yeye hatuwezi neno lolote.
Sisi  si maarufu  kuliko Mungu;  wala sisi si bora kuliko wengine.hatuna haja ya kuwa wabishi pasipo sababu ,kuwa wenye viburi ,wasiotaka kubadirika mm Fredrick sylvanus ninaungana na wewe rafiki Mpendwa tushushe kiburi cha uzima tusisubiri kupata mapigo ndipo tujishushe ,leo nnakuarika Mpendwa ujitoe kwa YESU ndiye anayefundisha tabia njema ,ndiye anayetoa kiburi ,anarudisha na kuumba upya tabia njema ,Karibu umpokee YESU atakuweka huru Bwana akubariki ,

Karibu kwa somo linalofuata.
Previous
Next Post »