HIVI MWISHO WA DUNIA UTAKUWAJE ?

HIVI MWISHO WA DUNIA UTAKUWAJE?

(SOMA  DANIELI  12  YOTE)

mwisho wa dunia ni nini ? Karibu kwa somo ninafuraha maana tunahitimisha kitabu cha Daniel usisite kurudia masomo yapo yote kwenye hii blog ,Bwana akubariki na azidi kukubariki zaidi katika maisha yako usipuuzie uliyojifunza . 

Mpendwa mfuatiliaji wa unabii huu yapo  mawazo  mengi  wanayosema  watu  kuhusu  mwisho  wa  dunia.    Wengine wanasema watakatifu watanyakuliwa kwenda mbinguni na  waovu wote wataangamizwa; dunia  itabaki  tupu.   Wengine  wanasema  kanisa  peke  yake  ndilo  litanyakuliwa;  watu waliobaki wataendelea kuishi duniani, na injili itahubiriwa kwa Wayahudi;  ndipo Mpinga Kristo atakuja na kufanya mambo yake.  
 Wengine  wanasema  mbinguni  watakwenda  tu wale 144,000, watu wengine wote waliobaki  makao yao ni hapa duniani;  na ya kwamba dunia hii haiwezi  kuharibiwa.    Kwa  hiyo  wanaangalia  majengo  mazuri na kusema  moyoni "Nitarithi  jumba  hili".   Je!   Biblia  inatupa  picha  gani  juu  ya  mwisho  wa  dunia?    
Na tunaposema tunaishi siku za mwisho tuna maana gani?  
Zilianza lini  kuhesabiwa?  

 Hebu Danieli atuambie katika Sura hii ya 12. Mwanzo wa siku za mwisho (Dan. 12:5-7):    Tunaona  kipindi  kile  kile  cha  Danieli 7:25 kinatajwa hapa  tena  na  "mtu  yule  aliyevikwa nguo  za kitani" [Kristo]  anayeonekana pia katika Ufu.  10:1-7.  Soma  pia Mt. 17:1,2;  Mk. 9:2,3.  Anasema  hivi,  "Itakuwa  wakati, na nyakati  mbili,  na  nusu  wakati;    tena  watakapokuwa wamekwisha  kuvunja nguvu  za hao watu  watakatifu,  ndipo  mwisho  wa  mambo  hayo  yote  yatakapotimizwa"  (fungu  la  7). Maneno hayo aliyatoa  akijibu  swali la mmoja  aliyemwuliza,  "Je!  itakuwa  muda wa miaka mingapi  hata  mwisho  wa  mambo  haya  ya  ajabu?  (fungu  la  6).    "Mambo  ya  ajabu"  ni mauaji  yaliyofanywa na  Upapa  katika Zama  zile  za Giza   ulipoua zaidi  ya  watakatifu milioni 50,  ambayo  yalimshangaza pia hata  Yohana  (Ufu. 17:6).   Kanisa  kuua  kanisa  ni ajabu  kuu!  Litakwenda mbingu ya nani? Nyakati 3 1/2 ni miaka 3 1/2 au miezi 42 au siku 1260 za unabii ambazo ni miaka 1260 ya Ufalme wa Papa wa Awamu ya Kwanza (538-1798).bila shaka hapa umepaelewa vizuri kwa masomo ya nyuma,    Kipindi  hicho  kimetajwa tena na tena katika unabii  (Dan. 7:25;  Ufu. 12:6,14;   13:5;  11:2,3;  Mt. 24:21,22).  Katika Dan. 11:33,34  anasema,  "...  wataanguka  kwa  upanga,  na  kwa  moto,  na  kwa kufungwa,  na kwa  kutekwa  nyara,  siku  nyingi  [538-1798].   Upapa  ulitumia  upanga,  moto,  kifungo, kuteka  nyara  kama  unabii  unavyosema  katika  kuwaua  watakatifu.    Mateso  yalikuwa mabaya mno kuliko ya  watu  wasiomjua Mungu.   Ufalme  wa  Papa ulioitawala  dunia  (Ulaya Magharibi) ulivunjwa na Wafaransa mapema mwaka 1798.  Kuanzia hapo fungu la Dan. 12:4 likaanza kutimia.  Maarifa ya kidini, kisayansi na kiteknolojia yaliongezeka kasi kwa namna  ya  ajabu.  
 Zama  za  Giza hazikuwa  na  maendeleo  yo  yote.   Wana-sayansi na Wanadini  waliofuata Biblia walikuwa wanauawa.   Mwaka  1798  ndio  mwanzo  wa "Siku  za  Mwisho".    Mwisho  wake utakuwa katika  Awamu  ya Pili  inayokuja ya Ufalme  wa Papa  -----   "tena  watakapokuwa  wamekwisha  kuvunja  nguvu  za  hao  watu  watakatifu" (Dan. 12:7).  Historia inajirudia yenyewe.  Mateso  na mauaji ya watakatifu  yatakuja tena atakapotawala Papa (Ufu.  6:9-11)    -----    "wakaambiwa  wastarehe  bado  muda  mchache, hata  itakapotimia  hesabu  ya  wajoli  wao  na  ndugu  zao,  watakaouawa  vile  vile  kama wao."  Wengi  hawaamini maneno hayo;   lakini wanapaswa  kungoja  mpaka yatakapotimia ndipo watakapoamini (Yoh. 14:29). Kusimamishwa kwa  Chukizo la  Uharibifu  au  Mwanzo  wa  Ufalme  wa  Papa  (Upapa):  Rumi ya Kipagani iliangushwa na makabila ya kipagani ya Ulaya Kaskazini mwaka 476 B.K.   Tangu  siku  za  Mfalme  Konstantino,  mwaka  330,  Askofu  wa  Roma  au  Papa aliachiwa  kutawala mji  wa  Roma.  
 Kwa  hiyo  Dola  ya Magharibi ya  Rumi  ilipoanguka, Papa aliendelea kutawala mji ule.  Alishika hatamu za utawala juu ya Ulaya Magharibi kuanzia mwaka  538  baada  ya  kuzing'oa  falme  tatu  -  Waheruli  (493),  Wavandali  (534),  na Waostrogothi (mapema 538).Mataifa yale mengine  ya Ulaya yalipokea  Ukatoliki kwa upanga  wa Mfalme Clovis wa  Ufaransa.   Kwa  hiyo,  yakajikuta  yako  tena  chini  ya  Papa,  (538-1798).    Clovis alifanikiwa kuyafanya Wakatoliki mwaka 508 (Dan. 12:11,12).  Kuanzia  mwaka  huo  wa 508  zinahesabiwa  siku  au  miaka  1290  na  1335.    Chukizo  la  Uharibifu  lilisimamishwa [lilitawala] kuanzia 538 - 1798 (yaani, miaka 508 + 1290 =  1798 barabara).  Mwaka  ule wa  1798  ukawa  ndio  mwanzo  wa  siku  za  mwisho.   Hukumu  ikawekwa  mbinguni kumpimia  adhabu  yake  mwaka  1844,  yaani,  mwisho  wa  miaka  ile  2300  ya  Dan.  8:14 (yaani, miaka 508 + 1335 =  1843-1844).  Mwaka ukianza tarehe  2  Januari  unamalizika katika mwaka unaofuata. Kuna  heri  gani  kwa  watu  watakaoufikia  mwaka  1844,  mwaka   ambao  Hukumu ilianza  mbinguni?   Wale  walio  na  hekima  "watajitakasa  na  kujifanya  weupe"  (Dan. 12:3,9,10);    tena  watasimama kama  Danieli  katika  "kura" yao,   yaani,  majina  yao  yatabaki katika  Kitabu  cha  Uzima  mbinguni  pamoja  na  watakatifu  wote  waliotangulia  (Dan. 12:13).   Isitoshe  heri  nyingine  ni  ile ya  kufufuliwa  katika ufufuo  wa pekee  (Dan.  12:2;   Ufu. 14:13) kwa wale wote walioshiriki kuihubiri Injili ya Milele kwa uaminifu  (Ufu.  14:6-12).  Injili hiyo  inayoitwa  "Ujumbe  wa Malaika  Watatu"  ilianza  kuhubiriwa  1840-1844 na  bado inahubiriwa.   Ufufuo wa  watakatifu  wote utafuata  mara  tu  baada  ya  ufufuo huo  wa mseto utakaokuwa  na  wale  waliomchoma  pamoja  na  wale  waliowatesa  sana  watu  wa  Mungu (Ufu. 1:7;  1 The. 4:16,17[18]).

Mwisho wa Dunia Utakuwaje?  

 Tumeona  jinsi Ufalme wa  Papa  ulivyotawala katika Awamu ya Kwanza (538-1798)  na  ya  kwamba  unakwenda  kutawala  dunia  tena.    Hiyo itakuwa ni awamu  yake ya pili na  ya mwisho.  Maangamizi  ndiyo yatakayokuwa mwisho wa Ufalme huo.  

Mfuatano  wa matukio ni huu   -----

 Papa atawala  awamu ya pili, mateso na mauaji ya watakatifu  yaanza  tena kwa kipindi  kifupi sana,   Kristo, Kuhani  wetu Mkuu, anamaliza kazi  yake  ya  Maombezi  katika  Hekalu  la  Mbinguni  na  kuufunga  mlango  wa kutubu  au  wa  rehema  kwa  tamko  la Ufu. 22:11.  Watu wa  Mungu wametiwa muhuri wa Mungu katika vipaji vya nyuso zao;  na watu wa Mnyama wamepata alama ya  mnyama vipajini mwao  na  katika  mikono  yao.    Wakati  wa  taabu  unaanza  (Dan.  12:1)  Mikaeli (Kristo)  anapotawazwa  (anaposimama)  katika  Jiji  la  Yerusalemu  juu;    pepo  za  vita zilizozuiwa  zaachiliwa  na  vita  inatapakaa  kila  mahali  ikileta  maafa  mengi(Ufu.  7:1-4), vimbunga na  maafa mengine  yanatokea, ndipo silaha  ya  Mungu  ya kutisha  sana  kwa wale walioikanyaga  Sabato  yake  itakapotumika  (Mapigo  7  ya  Ufunuo  16).    Wale  wote watakaomfuata Papa majina yao  yataondolewa  katika  kitabu  cha  uzima  (Kut.  32:32,33;  Ufu. 13:8).  Mtihani wa siku za mwisho ni Amri ya Nne [Sabato](Ufu. 3:10; 14:9,10). Mchezo  wa  kuiweka  Jumapili  badala  ya  Sabato  [Jumamosi]  utakuwa  na  athari mbaya  mno  kwa  dunia  nzima  (Isa.  24:1-6,19,20;  Ufu.  19:11-21).    Ole  kwa  wafalme  wa dunia  hii!   Ole  kwa kila  mtu  asiyesimama upande  wa Yesu  Kristo katika  Pambano hili  Kuu! Karibu sana  litafikia  mwisho  wake.   Watoto  wa  Mungu  wamechoka  na dunia  hii  wanataka kwenda kupumzika mbinguni kwa miaka 1000, na Yesu anasema.

 " Tazama,  naja  upesi, na ujira wangu  u pamoja nami,  kumlipa  kila mtu kama  kazi yake ilivyo"  (Ufu.  22:11).  

Je! u tayari kumlaki  Bwana?
  Je!   utasimama  imara hata  kama mbingu  zikianguka,  na  kuiinua juu Bendera ya Imanueli [Kristo] iliyoandikwa  "Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao Amri [Kumi] za Mungu, na Imani ya Yesu" (Ufu. 14:12).    Hivi  karibuni dunia  hii  itabaki  tupu,  ndugu  yangu.   Kuanzia  leo  chagua  kuingia  Paradiso  pamoja  na Kristo (Luka 23:42,43;  2 Kor. 6:2).   Huenda usisikie  mwito mwingine  kama  huu.   Amua leo!
Ninakukaribisha uendelee kufuatilia unabii wa kitabu cha ufunuo ambao muda sio mrefu tutaanza kujifunza .
Pia unaweza kuandika uhuruhatimaye. blogspot. com kwenye search engine yeyote utayapata masomo bila shida ninakuomba Mpendwa ufanyapo mambo yako yote kumbuka pia YESU Kristo atarudi kwaajili yako kwahiyo jiandae kumpokea ajapo mala ya pili.Bwana akubariki sana.
Previous
Next Post »